KUKU WA NYAMA (BROILERS)
Kuku hawa hufugwa kwa madhumuni ya kupata nyama tu. Kuku hawa wanaweza kutaga mayai iwapo watawekwa mpaka wafike wakati wa kutaga, lakini hutoa wastani wa mayai 170 kwa mwaka, ambayo hayatamletea faida mfugaji akilinganisha na gharama za matunzo ya kuku huyo kufikia muda wa kutaga. Tanzania wapo kuku aina Anak, Cobb na Chunk
KUKU WA MAYAI
Kuku hawa ni wadogo kwa umbile na hutaga wastani wa mayai 230 kwa mwaka. Kuku wa mayai wamepoteza uwezo wao wa kulalia mayai na kuangua vifaranga. Kwa sababu hii wanapoanza kutaga huendelea kwa muda wa mwaka na zaidi iwapo watapewa mazingira yanayohitajiwa. Kuku mashuhuri na anayefahamika sana katika kundi hili ni Yule kuku mweupe anayefahamika kwa jina la white leghorn.
KUKU KWA AJILI YA MAYAI NA NYAMA
Kuku hawa ni wakubwa kuliko kuku wa mayai, lakini ni wadogo kuliko kuku wa nyama. Utagaji wao ni wastani wa mayai 212 kwa mwaka. Wastani huu wa mayai unaweza kumpatia faida mfugaji. Baada ya kutaga wanaweza kutumiwa kwa nyama kwa sababu wanakuwa na umbile kubwa.
Mfano wa kuku wa mayai na nyama ni Rhode Island Red ambaye ni kuku mwekundu. Kuku aina ya Light Sussex ambaye ni kuku mweupe na mwenye manyoya meusi shingoni, mkiani na kwenye mabawa, pia hutumika kwa nyama na mayai. Katika kundi hili la kuku wa nyama na mayai kuku aina ya New Hampshire na Australop pia huonekana nchini Tanzania. New Hampshire ni kuku mwekundu wastani na Australop ni kuku mweusi.
SOURCE:
- Kirumbi, D.M. (1980) Ufugaji wa Kuku (Dar es Salaam: Tanzania Publishing House)
No comments:
Post a Comment